Pichani ni Bwana Lilah Hussen alieungua vibaya mwili mzima akiwa ndani ya Ambulance ya hospitali ya Kigamboni tayari kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mara baada ya kuchomwa moto na walinzi pamoja na meneja wa hoteli ya South Beach iliopo kigamboni alipobainika kuwa aliingia hotelini hapo bila kulipa kiingilio.
Na Mdau Pius Micky wa Spoti na Starehe
Kijana mmoja aliefahamika kwa jina la Lilah Hussen,amechomwa na moto mwili mzima na walinzi wa Hotel ya South Beach wakishirikiana na Meneja mmiliki wa Hotel hiyo aliejulikana kwa jina moja la Shipata.
Tukio hili ambalo ni la kusikitisha sana,limetokea jana mchana katika hoteli hiyo. Wakiongea na mwahabari wetu, ndugu wa majeruhi huyo wamesema kuwa ndugu yao alifika ufukweni hapo ambapo kila mwisho wa wiki panakuwa na muziki kwa ajili ya kujiburudisha na alipoingia ndipo alipokamatwa na walinzi kwa kutokuwa na alama maalumu ambayo huvaliwa mkononi kwa waliolipa kiingilio cha hotelini hapo (kiingilio ni Tsh. 7,000/- kwa mtu) ndipo walinzi hao walipochukua jukumu la kumpeleka kwa Meneja wa Hoteli hiyo na ndipo meneja huyo alipoamrisha kijana huyo avishwe mipira na kuchomwa moto.
Bwana Lila ambaye kwa sasa kahamishiwa Hospitali ya Rufaa Muhimbili amesema yeye ni mfanyabiashara ndogo ndogo na mkazi wa Kigamboni na kuwa alikwenda hapo baada ya kuvutiwa na muziki pasi kujua kama hayo yaliyofanyika hapo yangemkuta.
Ndugu wa majeruhi huyu wamefungua kesi katika kituo cha Polisi Kigamboni lakini hadi hivi sasa na kwa masikitiko wanasema bado hatua zozote za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya wahusika wa tukio hilo kitu ambacho kinazidi kuwasikitisha ndugu hao wa majeruhi. Ufukwe wa hoteli ya South Beach umekuwa ukijizolea umaarufu kwa michezo ya ufukweni lakini wananchi wa kawaida ambao wanaishi eneo hili wamekuwa wakilalamikia ada kubwa ya kiingilio ufukweni hapo ikiwa ni Tsh. 7,000/- ada ya kuingia tu bila kinywaji.
Hivyo inafanya wakazi wa maeneo hayo watamani kufika mahala hapo lakini kutokana na gharama za kiingilio kuwa kubwa inawabidi waishie kusikia sifa tu toka kwa watu waendao mahala hapo.
Kijana Lilah kwa sasa yuko Hospitali ya Muhimbili akiendelea kupata matibabu kwani hali yake ilikuwa ni mbaya sana. Jeshi la Polisi mnaombwa kuliangalia swala hili kwa kina na ikiwezekana hatua za haraka za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wahusika waliofanya jambo hili ambalo ni la kinyama kabisa kwani hili si jambo la kulifumbia macho hata kidogo.
Habari na picha kwa hisani ya Othmani Michuzi.